BARAZA LA MADIWANI WILAYA YA BARIADI LATILIA MKAZO UKUSANYAJI WA MAPATO
Posted on: November 4th, 2022
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi limewasisitiza watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji na kata kuhakikisha wanakusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali vilivyopo katika Halmashauri hiyo.
Msisitizo huo umetolewa katika kikao cha Baraza la madiwani wakati wa kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo Robo ya Kwanza Julai - Septemba 2022/2023 kikao kilichofanyika Dutwa Wilayani Bariadi.
Mwenyekiti wa Baraza hilo Mh. Mayala Shiminji alibainisha kuwa msingi mkuu wa uendeshaji wa shughuli zote katika halmashauri yoyote ni mapato hivyo kwa namna yoyote watendaji ambao wanahusika moja kwa moja na ukusanyaji wa mapato lazima wahakikishe vyanzo vya mapato vilivyopo vinasimamiwa ipasavyo na vinaleta tija.
Mh. Mayala alibainisha kuwa awali waliweka makubaliano ya kugawana jukumu la ukusanyaji wa mapato ambapo vipo vyanzo vilisimamiwa na kukusanywa na ngazi ya kata na vyanzo vingine vilisimamiwa na kukusanywa na timu ya mapato ngazi ya Halmashauri.
Timu ya mapato katika kipindi cha robo ya Julai - Septemba 2022/2023 wamekusanya kiasi cha Shilingi Milioni 556.9 sawa na asilimia 75 ya mapato yote yaliyokusanywa katika robo ya kwanza jambo ambalo lilipongezwa na Mwenyekiti huyo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Bariadi Bi. Juliana Mahongo pamoja na kutoa pongezi kwa Waheshimiwa Madiwani pamoja na wataalamu kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuiendeleza Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi lakini hakuacha kuelezea umuhimu wa ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Halmashauri.
“Suala la mapato si maombi, ni lazima mapato yakusanywe ili Halmashauri hii iwe na mipango yake thabiti na isiwe Halmashauri omba omba” alisisitiza Bi. Mahongo
Baraza hilo pamoja na kupitia na kujadili taarifa za maendeleo za kata na taarifa za kamati pia walipokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali kutoka taasisi na mamlaka kama vile TARURA, TANESCO na RUWASA hivyo kuwapa fursa Waheshimiwa madiwani kutoa michango yao juu ya mienendo ya utekelezaji wa miradi hiyo.