Bariadi, 14 Januari 2026 —
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi leo imefanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, kikilenga kupitia na kujadili rasimu ya mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Kikao hicho kilihusisha wajumbe kutoka Vyama vya Wafanyakazi, Wakuu wa Vitengo na Idara za Halmashauri pamoja na wawakilishi wa watumishi, ambapo hoja mbalimbali za ustawi wa watumishi na uendeshaji wa Halmashauri zilijadiliwa kwa kina.
Moja ya hoja muhimu iliyojadiliwa ni jitihada zinazofanywa na Halmashauri katika kulipa madeni ya watumishi. Iliainishwa kuwa kwa mwaka 2025, jumla ya shilingi 83,510,180 zimelipwa kwa watumishi wasio walimu 75, huku shilingi 9,556,366.80 zikilipwa kwa wastaafu 19. Fedha hizo zote zimetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE, Bi. Catherine Nyingi, alipongeza jitihada za Halmashauri katika kulipa madeni hayo, huku akihoji sababu ya baadhi ya watumishi kuendelea kulalamikia madeni ya muda mrefu na kama kuna uwezekano wa wao kulipwa.
Akijibu hoja hiyo, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Rasilimali Watu, Bi. Shakira Hamis, alisema kuwa changamoto kubwa imekuwa ni baadhi ya watumishi kushindwa kufuata taratibu za kuwasilisha madai yao kwa maandishi kama inavyotakiwa. Alisisitiza kuwa watumishi wenye madai wanapaswa kuzingatia taratibu hizo ili kuwezesha madai yao kushughulikiwa na kulipwa kwa wakati.
Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa kikao hicho, Ndg. Kenedy Mhina, alisema tangu aanze kuhudhuria vikao vya Baraza la Wafanyakazi amekuwa akitiwa moyo na namna maazimio ya baraza hilo yanavyotekelezwa na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa watumishi.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi kama jukwaa la kujenga mshikamano, uwazi na ushirikishwaji katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo, huku kikiweka msingi imara wa kuboresha ustawi wa watumishi na ufanisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.