MRADI WA MAJI WA BILIONI 440 KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI SIMIYU.
Posted on: January 10th, 2025
Mradi wa ujenzi wa Bomba la maji kutoka ziwa Victoria kuja mkoa wa Simiyu unatarajiwa kumaliza changamoto ya maji katika maeneo mengi ya Mkoa wa Simiyu.Akifafanua suala hilo wakati wa ziara ya kijiji kwa kijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mhe.Kenani Kihongosi amefafanua kuwa mradi huo mkubwa upo katika hatua nzuri ya utekelezwaji ambapo kwa awamu ya kwanza mradi huo utatekelezwa Wilaya ya Busega, Bariadi na Itilima kisha Wilaya ya Maswa na Meatu.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika mkoa wenu huu wa Simiyu ametupatia fedha Bilioni 440 ziende kutoa maji ziwa victoria zisambaze mkoa mzima wa Simiyu. Katika Wilaya hii ya Bariadi tayari kuna matanki makubwa yanajengwa, Bariadi hapa kuna tanki la Lita Milioni 6 limejengwa na limekamilika,ukienda Itilima kuna tanki la Milioni 10 na tanki la Milioni 12 kwahiyo hii kero ya maji mpaka Desemba mwaka huu maji yatakuwa yakutosha ndani ya Mkoa wa Simiyu.” alifafanua Mhe.Kihongosi
Ziara ya Mhe.Kihongosi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ni mwendelezo wa ziara yake kijiji kwa kijiji ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi ambao mamia ya wananchi hao wamejitokeza ili kuwasilisha kero zao kwaajili ya kupatiwa ufumbuzi.