MWENYEKITI WA TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI AONGOZA KIKAO CHA KUJIRIDHISHA JUU YA MAOMBI YA KUGAWA JIMBO LA BARIADI
Posted on: April 24th, 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo Aprili 24, 2025 ameongoza kikao cha pamoja kati ya Tume na wadau wa uchaguzi Wilaya ya Bariadi ili kujiridhisha juu ya maombi yaliyowasilishwa ya kugawa Jimbo la Bariadi kuwa majimbo mawili.
Akifafanua katika kikao hicho Mhe.Jaji Mwambegele alieleza kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea maombi ya kuligawa Jimbo la Bariadi ili yawe majimbo mawili ambapo katika maombi hayo wadau walishauri kuwa Jimbo moja liitwe 'Bariadi Mji' ambalo litakuwa na jumla ya Kata 10 na Jimbo la 'Bariadi Vijijini' ambalo litakuwa na Kata 21.
Aidha katika kikao hicho Mhe.Jaji Mwambegele aliwauliza wadau hao endapo maombi ya kuligawa Jimbo la Bariadi yaliyowasilishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu ni sahihi na kama yamefata taratibu za vikao vyote vya kisheria ndipo wadau hao kwa ujumla wao walikiri maombi hayo kuwa ni sahihi na yamefata taratibu za kujadiliwa kwenye vikao vya kisheria.
Wadau walioshiriki katika kikao hicho wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na viongozi wa asasi za kiraia walipongeza uanzishwaji wa mchakato huo kutokana na uhalisia kwamba Jimbo la Bariadi ni kubwa kieneo na ni Jimbo pekee lenye Halmashauri mbili hivyo kuligawa kutarahisisha usimamizi wa shughuli mbalimbali za maendeleo.