Bariadi, Februari 3, 2026
Meneja wa Benki ya NMB Tanzania, Tawi la Bariadi Mjini, Ndg. Andrew Msonga, leo Februari 3, 2026, ameongoza timu ya wataalamu wa Mikopo na Mahusiano ya benki hiyo kufanya ziara na mazungumzo na Menejimenti ya Kamati ya Ushauri ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika ndani ya ukumbi mdogo wa Halmashauri, Ndg. Msonga ametoa shukrani za dhati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kwa ushirikiano mzuri walioutoa kwa Benki ya NMB katika mwaka 2025, hususan katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia watumishi na wadau mbalimbali kwa ufanisi.
Amesema pamoja na kuwasilisha salamu za heri ya mwaka mpya, lengo kuu la ziara hiyo ni kuujulisha uongozi wa Halmashauri kuwa Benki ya NMB Tanzania imeamua kurejesha gawio la TSh milioni 750 kwa jamii na wadau wake kama ishara ya shukrani kwa ushirikiano na mchango wao katika ukuaji wa benki na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Ndg. Msonga, gawio hilo litalenga kusaidia sekta muhimu za kijamii ikiwemo elimu, ambapo shule zitanufaika kwa kupatiwa madawati; sekta ya afya kwa kupatiwa vifaa tiba, hususan vinavyohusiana na huduma za uzazi; pamoja na utekelezaji wa programu maalum ya ufadhili wa elimu iitwayo “ *Nuru Yangu”* , inayosaidia wanafunzi kuanzia ngazi ya sekondari hadi elimu ya juu.
Ameeleza kuwa kupitia programu ya Nuru Yangu, jumla ya wahitimu wa vyuo 21 waliweza kuajiriwa mwaka huu, hatua inayoonesha mchango wa NMB katika kuendeleza rasilimali watu na kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana. Aidha, sehemu ya gawio hilo itatumika kukamilisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa masoko na stendi, kusaidia waathirika wa majanga ya asili, pamoja na kutoa msaada katika nyakati za mitihani na mahitaji mengine ya kijamii.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg. Steven Masunga, aliuliza kuhusu namna ambavyo NMB itaweza kusaidia changamoto ya upungufu wa madawati unaojitokeza kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza katika shule nyingi wilayani humo. Pia alieleza kuhusu mwanafunzi mmoja aliyefanya vizuri katika Mtihani wa Darasa la Saba na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha, lakini anatoka katika familia isiyo na uwezo, hali iliyosababisha Halmashauri na Baraza la Madiwani kumchangia ili aweze kuanza masomo.
Akijibu hoja hizo, Ndg. Msonga amesema kuhusu upungufu wa madawati, walimu wakuu wanapaswa kuandaa maandiko rasmi na kufuata taratibu zilizowekwa ili benki iweze kupitia na kuona namna bora ya kushiriki katika kutatua changamoto hiyo. Kuhusu mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha, Meneja huyo amesisitiza kuwa taratibu za kuomba ufadhili zinapaswa kufuatwa kwa kujaza maombi kupitia mfumo wa mtandao kama itakavyoelekezwa rasmi.
Ameongeza kuwa Benki ya NMB ni mdau mkubwa wa Serikali katika kuunga mkono maendeleo ya nchi, ikichangia takribani asilimia 30.7 ya mapato, hali inayoonesha dhamira ya benki hiyo katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mbali na ujumbe kuhusu gawio la TSh milioni 750, wataalamu wa NMB waliotembelea Halmashauri hiyo pia walitoa elimu kwa viongozi kuhusu masuala ya mikopo, uwekezaji na matumizi sahihi ya "credit card", ikiwa ni sehemu ya juhudi za benki hiyo katika kuongeza uelewa wa kifedha kwa wadau wake.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha dhamira ya Benki ya NMB kuendelea kushirikiana na Serikali na Halmashauri za Wilaya katika kusukuma mbele maendeleo ya jamii na ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Bariadi na Taifa kwa ujumla.
#NMB #NMBKwaJamii #Maendeleo #Elimu
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.