Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu wawili (2-in-1) katika Shule ya Msingi Senta, iliyoko Kijiji cha Senta, Kata ya Masewa. Mradi huu umefikia hatua ya ukamilishaji kwa asilimia 95, ikiwa ni ishara ya jitihada madhubuti za kuboresha mazingira ya kufundishia na kuishi kwa walimu.
Ujenzi huu unatekelezwa kwa kutumia fedha kutoka Serikali Kuu zilizopokelewa tarehe 03 Septemba 2024 kupitia Programu ya Global Partnership for Education – Teachers Support Program (GPE–TSP), kiasi cha shilingi milioni 100. Lengo kuu la GPE–TSP ni kuboresha ustawi wa walimu kwa kuwapatia makazi ya uhakika, jambo linalotarajiwa kuongeza ufanisi wao kazini na kuchochea matokeo bora ya elimu kwa wanafunzi.
Kupitia mpango huu, walimu wa Shule ya Msingi Senta watanufaika kwa kuishi karibu na shule, hali itakayorahisisha utendaji wao wa kila siku na kukuza ari ya kufundisha.
Katika mwaka wa fedha 2022/23 na 2023/24, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia programu mbalimbali kama BOOST na SEQUIP, imewezesha ujenzi wa nyumba 860 za walimu (shule za msingi na sekondari), zikinufaisha jumla ya familia 2,018. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 263 za walimu katika shule za msingi pekee.
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi inaendelea kushukuru Serikali kwa uwekezaji endelevu katika sekta ya elimu, hususan katika kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu, ambao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya elimu nchini.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.