Kamati ya Elimu, Afya na Maji ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, tarehe 22 Januari 2025, ilifanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa wodi ya watoto katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya afya katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Mganga Mfawidhi wa Wilaya, Ndg. Magembe Kuligwa Pelana, alibainisha kuwa kiasi cha Tsh 172,000,000 kilitolewa kwa hospitali hiyo kwa ajili ya kukamilisha Wodi Ya Watoto, Jengo la Upasuaji, na Jengo la kuhifadhi Maiti. Kati ya fedha hizo, Tsh 59,828,767 tayari zimetumika kwa wodi ya watoto.
Mradi huo, unaosimamiwa na mkandarasi, umefikia hatua za mwisho za ukamilishaji, ikiwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya maji safi, maji taka, umeme, na kufunga milango pamoja na madirisha ya vioo. Ujenzi unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo tarehe 2 Februari 2025, ambapo huduma kwa watoto zitaanza kutolewa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Jonas Nyaena, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa msaada mkubwa wa serikali katika kufanikisha miradi ya maendeleo. Pia aliwashukuru wataalamu wote kwa jitihada za kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa jamii.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imeidhinisha Tsh 472,000,000 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali hiyo, hatua inayotoa matumaini makubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Bariadi.
Ujenzi wa wodi ya watoto ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya, hasa kwa watoto, na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.