Mnamo tarehe 23 Januari 2025, Kamati ya Uchumi, Ujenzi, na Mazingira ilifanya ukaguzi wa Mradi wa Kitalu cha Miti uliopo katika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi. Mradi huu unaofadhiliwa na Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa Mkoa wa Simiyu (SCRP) pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, umefanikiwa kutokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Misitu Wilaya, Bi Bahati Pius, mradi huu umepokea ufadhili wa Tsh. 1,925,400/= kutoka SCRP kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, na Tsh. 2,039,000/= kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya shughuli za kujaza viriba, ununuzi wa mbegu, uvutaji wa maji, na huduma za kitalu. Hadi sasa, mradi umegharimu jumla ya Tsh. 3,964,400/=.
Shughuli za kuandaa kitalu zilianza tarehe 20 Oktoba 2024, zikilenga kuotesha miche 20,000 ya kivuli (19,250) na matunda (750). Licha ya changamoto kama mifugo kula miche na ukame, uotaji wa mbegu umefikia asilimia 90, jambo linalodhihirisha maendeleo mazuri ya mradi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Duka Mashauri Mapya, alitoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Halidi M. Mbwana, na wataalamu wote kwa juhudi zao. Tangu kuanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri imeweza kusambaza miche 204,458 kwa taasisi mbalimbali, zikiwemo shule na vituo vya afya.
Mradi huu unaonyesha umuhimu wa usimamizi bora na ushirikiano katika jitihada za hifadhi ya mazingira, huku ukiwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.