WAFUGAJI WASISITIZWA KUJIANDAA NA CHANJO YA MIFUGO MACHI, 2025
Posted on: February 6th, 2025
Wafugaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wamesisitizwa kujiandaa na chanjo ya mifugo inayotarajiwa kuanza Mwezi Machi mwaka huu ikiwa ni juhudi za Serikali kuhakikisha tija inapatikana katika sekta ya Mifugo.
Kaimu Mkurugenzi Bariadi DC Mhandisi.Wilbert Siogopi akifafanua kuhusu chanjo ya mifugo
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika leo Februari 06, 2025 kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mhandisi Wilbert Siogopi ameeleza kuwa chanjo hiyo itahusisha ng'ombe, mbuzi, kondoo na kuku ikiwa na lengo la kukinga mifugo dhidi ya magonjwa ya homa ya mapafu kwa ng'ombe, sotoka kwa mbuzi na kondoo pamoja na Kideri kwa kuku.
Mhandisi Siogopi aliendelea kufafanua kuwa Serikali imetoa ruzuku katika upatikanaji wa chanjo hiyo hivyo gharama itapungua ambapo kwa ng'ombe mmoja chanjo itakuwa ni shilingi 500, Kwa mbuzi na kondoo mmoja itakuwa shilingi 300 na kwa kuku itakuwa ni bure badala ya shilingi 100 ya awali.
Waheshimiwa Madiwani (waliovaa kaunda suti) wakiwa katika mkutano wa Baraza la Madiwani
"Wizara itagharamia ununuzi wa chanjo na mgao wa chanjo hizo utafanyika katika Halmashauri zote kwa kuzingatia idadi ya mifugo katika Halmashauri husika,Mheshimiwa Mwenyekiti makusanyo yote yatafanyika kwa kupitia POS hivyo kila mdau anawajibu wa kufanikisha zoezi hili la kitaifa kwani ni zoezi la lazima na sio hiari" alisisitiza Kaimu Mkurugenzi huyo.