Bariadi, Juni 20, 2025 —
Mwenyekiti wa Baraza Maalum la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mayala Shiminji, amefungua rasmi mkutano wa baraza hilo kwa shukrani na pongezi kwa madiwani na wataalam kwa usimamizi mahiri wa miradi ya maendeleo ndani ya miaka mitano iliyopita.
Katika hotuba yake, Mhe. Shiminji alieleza kuwa lengo la kikao hicho ni kupokea taarifa ya majibu ya hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024, sambamba na kusherehekea mafanikio yaliyopatikana kwa ushirikiano wa pamoja.
“Tumefanikisha ujenzi wa zahanati 11, vituo vya afya viwili (Matongo na Miswaki), shule za sekondari 8, shule za msingi 15, upatikanaji wa umeme vijijini kupitia REA, mradi wa maji wa Ziwa Victoria, visima vikubwa, barabara, madaraja, na mradi wa bwawa la umwagiliaji Kasoli ambao umepokea zaidi ya Tsh bilioni 11,” alisema Shiminji.
Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru madiwani na wataalam kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Simiyu, mradi uliomgusa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuipa heshima Mkoa wa Simiyu.
“Kwa kweli mmetusimamisha kwa uaminifu na umakini mkubwa. Nawapongeza wote kwa kazi nzuri, miradi imekamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa,” alihitimisha.
#bariadidc
#CAG
#MkoaSimiyu
#BarazalaMadiwani
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.