Mradi wa Maji Sapiwi, uliogharimu kiasi cha Shilingi milioni 769.4 fedha kutoka Serikali Kuu, umezinduliwa rasmi tarehe 13 Agosti 2025 na Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika Kijiji cha Sapiwi, Kata ya Sapiwi, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu.
Mradi huu, ambao ulizinduliwa kwa jiwe la msingi mnamo tarehe 05 Agosti 2024 na Ndg. Godfrey Eliakimu Mnzava, unalenga kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Vijiji vya Sapiwi na Mwandama pamoja na vitongoji vyake.
Kwa sasa, mradi unazalisha lita 158,400 za maji kwa siku, ukikidhi mahitaji ya takribani 6,865 wananchi sawa na asilimia 80.3 ya wakazi waliokusudiwa kuhudumiwa. Hadi kufikia Juni 2025, jumla ya lita 10,698,000 zimezalishwa na kusambazwa kupitia ‘DP’ 16 zilizowekwa, huku kaya 56 zikifaidika moja kwa moja kwa kuunganishwa na huduma ya maji majumbani.
Kiasi cha fedha kilichokusanywa kutokana na huduma hii ni Sh. milioni 23.8, ambapo matumizi ya uendeshaji na matengenezo yaligharimu Sh. milioni 21.8. Ili kudumisha uendelevu wa mradi, wananchi wamepewa elimu ya matumizi sahihi ya maji na ulinzi wa miundombinu, huku Kamati ya Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSO – SAMA) ikisajiliwa kwa usimamizi wa kila siku.
Mradi wa Maji Sapiwi ni miongoni mwa hatua muhimu zinazosaidia kufanikisha Ajenda ya Taifa ya Maji kwa Wote ifikapo 2030 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ukiwa chachu ya kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.