Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon P. Simalenga, leo tarehe 13 Oktoba 2025, amekabidhi jumla ya trekta 26 kwa waendeshaji (opereta) wa wilaya hiyo kwa ajili ya kuanza msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2025/2026.
Hafla hiyo imefanyika katika Mtaa wa Nyasosi, ndani ya Halmashauri ya Mji Bariadi, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imepokea trekta 21 zitakazogawanywa katika kila Kata ili kusaidia kulima mashamba ya wakulima wa pamba.
Kupitia mpango huo, wakulima watatozwa gharama ya Shilingi 35,000 tu kwa ekari moja, ambapo sehemu ya gharama nyingine inalipwa na Serikali kama ruzuku kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa pamba.
Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mhe. Simalenga alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kilimo ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi na sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa wilaya.
“Tunataka kuona kila mkulima ananufaika na kazi yake. Serikali imeleta trekta hizi ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato cha wakulima wetu,” alisema Mhe. Simalenga.
Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania kuimarisha kilimo cha pamba, kuongeza uzalishaji, na kuinua uchumi wa wananchi wa Bariadi na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla.
#BariadiYajitegemea #KilimoBora #PambaNiDhahabu #DCBariadi #Simiyu
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.