Kikundi cha Vijana Wachapakazi kutoka Kijiji cha Banemhi, Kata ya Banemhi, kimeendelea kuonyesha mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022.
Kikundi hiki chenye wanachama sita (wote wanaume) kilisajiliwa rasmi tarehe 28 Aprili 2022 kwa Namba CD/BRD/CBO/1006, na kimekuwa mfano wa utekelezaji bora wa mikopo ya vijana inayotolewa na Halmashauri kupitia Mfuko wa Vijana 4%.
Mradi huu, ambao ulizinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa tarehe 05 Agosti 2024 ukiongozwa na Ndg. Godfrey Eliakimu Mnzava, umegharimu jumla ya Tsh. milioni 20. Kati ya hizo, Tsh. milioni 2 zilitokana na mchango wa wanakikundi na Tsh. milioni 18 ni mkopo wa Halmashauri.
Kupitia shughuli za usafirishaji (bodaboda), wanakikundi wote sita wamepata ajira ya kudumu, huku baadhi yao wakiweza kuboresha makazi na kushiriki katika huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya. Aidha, mradi huu umehamasisha vijana wengine kuanzisha vikundi vya kiuchumi kupitia mikopo ya mapato ya ndani.
Hadi sasa kikundi kimefanikiwa kurejesha Tsh. milioni 13.6 ndani ya mwaka mmoja, na kimesalia na deni la Tsh. milioni 4.4 pekee.
Ili kuhakikisha mradi unakuwa endelevu, vijana hao wameweka mikakati ya kupata mafunzo ya ujasiriamali, kuanzisha mfumo wa kumbukumbu za mapato na matumizi, kutenga sehemu ya mapato kwa matengenezo na upanuzi wa mradi, pamoja na kuimarisha ushirikiano na Halmashauri kwa msaada wa kitaalamu.
Mradi wa Vijana Wachapakazi Banemhi unatajwa kuwa mfano bora wa utekelezaji wa sera za Serikali kupitia mikopo ya Mfuko wa Vijana (4%), inayolenga kuwawezesha vijana kujitegemea, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.