Bariadi, Simiyu – Aprili 30, 2025:
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi inatarajia kuanza kutoa dozi ya pili ya chanjo ya sindano ya polio (IPV2) kwa watoto kuanzia mwezi Mei 2025, kama hatua ya kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa kupooza kwa watoto walio katika hatari zaidi.
Hayo yamesemwa katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kilichofanyika tarehe 29 Aprili 2025 katika Makao Makuu ya Halmashauri hiyo. Akizungumza na wajumbe wa kikao hicho, Mratibu wa Chanjo Wilaya, Ndg. Abdulazizi Ramadhani, amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa polio katika nchi jirani zikiwemo Malawi, Zambia, Burundi na Congo.
"Kutokana na mwingiliano wa wananchi baina ya Tanzania na mataifa haya, kuna hatari ya maambukizi ya virusi vya polio. Chanjo hii ya pili inalenga kuongeza kinga kwa watoto walio na umri wa miezi tisa," alisema Ndg. Ramadhani.
Ameeleza kuwa ugonjwa wa polio unasababishwa na virusi vya Poliovirus vinavyoweza kuingia mwilini kupitia chakula au maji machafu, na baadaye kushambulia mishipa ya fahamu, hivyo kusababisha kupooza. Alibainisha kuwa dozi ya kwanza ya sindano ya polio (IPV) hutolewa mtoto anapofikisha wiki 14, na kwamba hii ni nyongeza ili kuimarisha kinga zaidi.
Katika kikao hicho, mmoja wa wazee maarufu kutoka Kijiji cha Igaganulwa, Bw. Amos M. Lubacha, alihoji kwa nini chanjo hiyo inalenga watoto pekee ikiwa ugonjwa huo ni hatari kwa wote. Akijibu swali hilo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Pilila Zambi, alieleza kuwa kwa sasa maelekezo ya Wizara ya Afya ni kutoa chanjo hiyo kwa watoto wa miezi tisa, na iwapo kutatokea mabadiliko, jamii itaelekezwa ipasavyo.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi wa kikao hicho ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bariadi, Ndg. Justine Manko, amewataka wajumbe wote kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo na hasa kinga dhidi ya ugonjwa hatari wa polio.
Wajumbe wa kikao hicho walihusisha Kamati ya Usalama ya Wilaya, wazee maarufu, viongozi wa kijadi na dini pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Kwa mara ya mwisho Tanzania iliripoti mgonjwa wa polio mwaka 1996, lakini kutokana na tishio la kurudi kwa ugonjwa huo duniani, serikali imeamua kuimarisha kinga ili kuzuia uwezekano wa maambukizi nchini.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.