BARIADI DC YABAINISHA SHUGHULI ZILIZOTEKELEZWA MWAKA 2024/2025
Posted on: December 17th, 2024
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi leo tarehe 17 Disemba 2024 imewasilisha taarifa ya mapitio ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambayo imeeleza shughuli na miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika kipindi cha nusu mwaka na inayoendelea kutekelezwa.
Akiwasilisha taarifa hiyo katika kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya (DCC) Afisa mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Ndg. Sayi Luseba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Bariadi alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 halmashauri ya wilaya ya Bariadi ilikisia kupata kiasi cha fedha Shilingi Bilioni 35.7 kutoka vyanzo mbalimbali kama vile mapato ya ndani shilingi bilioni 2.5 ruzuku toka serikali kuu (OC) bilioni 2.1 mishahara bilioni 22.9 na miradi ya maendeleo bilioni 8.
Miongoni mwa shughuli na miradi inayotekelezwa ni pamoja na kuchangia kiasi cha shilingi milioni 33.2 kwaajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 400 kwaajili ya jengo la upasuaji na wodi mbili za upasuaji katika hospitali ya Wilaya ya Bariadi. Kutoa fedha za ruzuku kwa kaya masikini 6,510 ambapo jumla ya shilingi milioni 953 zimelipwa kwa walengwa hao pamoja na ujenzi wa shule mpya mbili za sekondari kata ya Nkololo moja ikiwa ni shule ya amali ambapo kila mradi una thamani ya shilingi milioni 584.
Ndg. Luseba alieleza pia changamoto mbalimbali ambazo zinazojitokeza katika utekelezaji wa mpango na bajeti wa mwaka 2024/2025 ambapo moja ya changamoto hiyo ni matumizi ya fedha nyingi katika kudhibiti wanyama wa kali ambao huvamia vijiji vilivyopo kandokando ya hifadhi.
kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya Bariadi kiliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Simon Simalenga na kushirikisha wadau mbalimbali kama vile wakuu wa Idara na vitengo kutoka halmashauri ya mji na halmashauri ya wilaya ya Bariadi, viongozi wa taasisi za serikali, viongozi wa vyama vya siasa, watendaji wa kata pamoja na viongozi wa dini ambao kwa ujumla wao waliweza kutoa michango yao katika mapendekezo ya mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.