"Taarifa hii inatoa picha ya maendeleo makubwa katika kuboresha huduma za afya ndani ya Wilaya ya Bariadi. Ujenzi wa Jengo la Upasuaji, Jengo la Kuhifadhi Maiti, na Wodi ya Watoto ni hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya bila changamoto kubwa za kusafiri umbali mrefu."
Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Bariadi, Ndg. Magembe Kuligwa Pelana, alibainisha haya tarehe 22 Januari 2025 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli zilizofanyika katika robo ya pili ya mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa Kamati ya Elimu, Afya, na Maji. Uwasilishaji huu ulifanyika ndani ya Jengo la Upasuaji lililo katika hatua za mwisho za ujenzi, wilayani Bariadi.
Taarifa yake ilihusisha mchanganuo wa matumizi ya shilingi milioni 172 zilizotolewa kwa ajili ya miradi mitatu ya afya, ikiwemo Jengo la Upasuaji, Jengo la Kuhifadhi Maiti, na Wodi ya Watoto. Alieleza pia hatua zilizofikiwa katika ujenzi, ni pamoja na kuunganisha mifumo ya maji safi, maji taka, umeme, na kufunga milango pamoja na madirisha ya vioo.
Aidha, Mganga Mkuu Wilaya, Ndg. Pilila Zambi alibainisha kuwa hospitali tayari imepokea vifaa vya thamani ya shilingi milioni 96 kwa ajili ya huduma za upasuaji, huku akitaja kuwa huduma rasmi katika wodi ya upasuaji zinatarajiwa kuanza tarehe 2 Februari 2025.
Mhe. Mwamba Madebele ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo,alisisitiza kuwekwa kwa vifaa kwenye wodi ya upasuaji na kuanza kwa huduma mara moja ili kuondoa usumbufu wa wananchi kulazimika kupata rufaa ya hospitali ya Mkoa. Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika ipasavyo.
Kamati ilitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine kwa juhudi za kufanikisha miradi ya maendeleo. Ushirikiano kati ya serikali kuu, viongozi wa wilaya, na wataalamu wa afya ni muhimu katika kufanikisha miradi kama hii.
Serikali imeidhinisha shilingi milioni 472 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo, jambo linaloonyesha dhamira ya serikali kuimarisha huduma za afya vijijini.
Kwa mwezi hospitali imekuwa ikifanya upasuaji wa wagonjwa kati ya 10%-17%, kukamilika kwa Jengo la Upasuaji na kuanza kutumika kwa huduma zake kutaboresha sana hali ya afya ya wananchi wa Bariadi. Hii pia itapunguza gharama na usumbufu wa kupata huduma za afya katika hospitali za mbali. Kwa kuzingatia hatua zilizofikiwa, ni muhimu kuendelea kusimamia mradi kwa uwazi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa viwango vinavyostahili.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.