DC BARIADI AFANYA KIKAO NA VIKOSI KAZI VYA PAMBA VYA KATA ZOTE
Posted on: May 11th, 2023
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mh. Simon Simalenga leo Mei 11 amefanya kikao na wajumbe wa vikosi kazi wa zao la Pamba vinavyojumuisha Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Kata, Maafisa Elimu kata, Maafisa Ugani, Watendaji wa Vijiji pamoja na Makatibu wa Amcos.
Mh.Simalenga alibainisha kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kujadili na kupeana maelekezo mbalimbali ambayo yatasaidia katika usimamizi wa ununuzi Pamba ambao utaanza rasmi hivi karibuni.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao kazi cha Mkuu wa Wilaya ya Bariadi
Miongoni mwa mambo ambayo Mh. Simalenga amesema yatafanyika katika msimu huu wa pamba katika Wilaya ya Bariadi ni pamoja na uhakiki na ukaguzi wa mizani mara kwa mara, uwekaji wa vizuizi vya ukaguzi wa pamba katika maeneo yote muhimu, kuzuia pamba kusafirishwa nyakati za usiku pamoja na kubainishwa kwa magari yote ambayo yatahusika na usafirishaji wa pamba ili kuepuka utoroshwaji unaofanywa na baadhi ya wanunuzi.
Aidha Mh. Simalenga amewaonya wanunuzi wote kutonunua Pamba chini ya bei iliyoelekezwa, kutowakopa wakulima na kutojihusisha na tabia za utoroshaji wa pamba kwani kufanya hivyo ni makosa kisheria na kamwe haitoivumilia kampuni yoyote itakayofanya vitendo hivyo.