"Serikali ya Tanzania kupitia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe alitoa ahadi kwamba Mhe. Rais analeta Trekta zaidi ya mia nne kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa pamba pamoja na mazao mengine, ili kulima kwa bei nafuu. Maelekezo yamekuja kwamba kwa heka moja trekta litatakiwa kumlimia mwananchi kwa kiasi kisichozidi tsh 35,000." Mhe. Simon P. Simalenga.
Haya yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Simon P. Simalenga,Jana tarehe 30/10/2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya, Isenge Dutwa. Amesema trekta yaliyopokelewa wilaya ya Bariadi ni 30 na kila Kata imekabithiwa trekta moja ambalo litasimamiwa na mwakilishi kutoka Bodi ya Pamba ya Wilaya.
Aidha ameongeza kuwa Bodi ya Pamba itaongeza matrekta mengine 10 na idadi kuwa trekta 40 kwa wilaya ya Bariadi, hivyo wakati matrekta hayo yakifika, viongozi wote wa Wilaya wa ngazi zote za Chama cha Mapinduzi na Serikali washirikishwe katika Mapokezi na Makabidhiano hayo.
Pia amesisitiza kuwa, kwa kuwa ugawaji wa Mbegu za Pamba umeshaanza maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenan Kihongosi kuhusu kutokugawa mbegu kwa mtu asiye na shamba au ambaye hajajiandikisha kwenye Daftari la Wakulima yanapaswa kuzingatiwa.Haitarajiwi mwaka huu kusikika kuwa kuna wananchi hawajalima pamba ila wamepewa mbegu za pamba na dawa kisha wanaziuza halafu uwiano wa mbegu na dawa zilizotolewa ukilinganisha na mavuno visiwe sawa itapelekea wahusika kuwajibishwa.
Mhe. Simon P. Simalenga alimalizia kwa kuwasihi Madiwani kuwa wanapaswa kutojihusisha kabisa na ugawaji wa mbegu za pamba na dawa za kuuwa wadudu.
Kwanzia mwanzo wa Mwezi Octoba Halmashauri imeshapokea Tani 1400 za mbegu ya pamba aina ya " UKM 08 iliyonyonyolewa manyoya (delented)",na inaendelea kusambazwa maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuanza msimu wa kilimo cha pamba tarehe 15/11/2024.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.