DC BARIADI ONGOZA MDAHALO IKIWA NI MAADHIMISHO YA SIKU YA MUUNGANO
Posted on: April 26th, 2025
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Simon Simalenga leo Aprili 26, 2025 ameongoza mdahalo uliokutanisha makundi mbalimbali kama vile wazee, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa, watumishi wa umma na wanafunzi huku akisisitiza umuhimu wa kutunza Amani ya nchi yetu hasa tukiwa tunaelekea kwenye zoezi la kitaifa la Uchaguzi Mkuu.
"Tulinde sana Amani yetu kwani ikitokea tumeipoteza hatuna nchi nyingine ya kukimbilia na kumbuka yanapotokea machafuko wanaoumia zaidi ni wanawake,wazee na watoto" alisisitiza Mhe. Simalenga
Aidha katika mdahalo huo washiriki mbalimbali walipata fursa ya kuchangia mada kuhusu maendeleo mbalimbali yaliyopatikana tangu kuwepo kwa muungano huu ambao umedumu kwa miaka 61 sasa.
David Lameck ni mmoja wa wazee maarufu walioshiriki mdahalo huu, ameeleza hali ilivyokuwa kwa upande wa miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Bariadi.
"Enzi hizo safari ya kutoka hapa Bariadi kwenda Mwanza ulikuwa unatumia siku nzima takribani masaa 12, ulikuwa huwezi kwenda na kurudi kutokana na changamoto ya barabara lakini leo hii barabara ni ya lami unaweza kwenda Mwanza na kurudi karibu mara nne" alifafanua Mzee huyo
Aidha washiriki waliochangia mada katika mdahalo huo walieleza faida mbalimbali za muungano wetu kama vile namna unavyoimarisha umoja wa kitaifa hivyo walisisitiza kuwa ni jukumu letu sote kuulinda na kuudumisha.