Bariadi DC, Simiyu
Katika uso wa kila mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Nkololo kuna tabasamu la matumaini ,furaha ya kweli ya kujisomea kwenye maktaba mpya ya kisasa, jengo lililosheheni ndoto na maarifa.
Kupitia ufadhili wa OPEC Fund chini ya Mradi wa TASAF, ndoto hii sasa ni halisi! Kwa gharama ya TSh milioni 92.4 fedha zilipokelewa tarehe 14 Machi 2023, na kazi ya ujenzi ikaanza rasmi tarehe 17 Mei 2023. Leo hii, maktaba hiyo imefungua milango kwa wanafunzi 80 kusoma kwa wakati mmoja katika mazingira safi, tulivu na ya kuvutia.
Maktaba hii si tu jengo la kuta nne, ni daraja la maarifa, ni mlango wa fursa, na ni chombo cha kubadilisha maisha. Hapa, wanafunzi wanajifunza kwa kina, wanajikuza kiakili, na wanaandika upya mustakabali wao wa kielimu.
“Kipindi cha nyuma ilikuwa vigumu wakati mwingine kupata utulivu wa kujisomea ukiwa darasani, au kupata kitabu fulani, lakini sasa ni rahisi,kupitia maktaba unaweza kupata utulivu wa kusoma na vitabu vingi,” anasema Maria Maduhu, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Nkololo.
Ujenzi wa maktaba hii ni sehemu ya jitihada endelevu za Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anasoma katika mazingira bora yanayochochea ubunifu na ufanisi wa kitaaluma.
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi imepokea miradi sita kupitia mfuko wa TASAF, ikiwemo ujenzi wa Zahanati, Nyumba za Watumishi, na mabweni ya wanafunzi ,hatua kubwa ya kuimarisha ustawi wa jamii.
Elimu ni mwanga – na Nkololo sasa inang'aa kama taa ya matumaini kwa vizazi vya leo na kesho!
---
#TASAF
#OpecFund
#ElimuKwanza
#BariadiDC
#MaktabaYaNdoto
#NguvuYaMaarifa
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.