Bariadi, Simiyu – Juni 10, 2025
Katika kuimarisha matumizi bora ya ardhi na kulinda ikolojia ya Serengeti, Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) limefadhili upimaji na utoaji wa hati milki 100 za kimila kwa wananchi wa makundi maalumu katika vijiji 18 vinavyopakana na Hifadhi ya Serengeti, Pori la Akiba Kijereshi na Pori la Akiba la Maswa, wilayani Bariadi.
Akizungumza wakati wa kikao maalum kilichofanyika katika Kijiji cha Ihusi, Mjumbe wa Kamati ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bi. Lucia Sweetbert, alisema kuwa shughuli hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango wa matumizi ya ardhi ulioanzishwa mwaka 2024, ikiwa ni pamoja na usimikaji wa vigingi katika maeneo mbalimbali ya kijiji.
Katika kikao hicho, Bi. Lucia alitoa utambulisho wa awamu ya pili ya mradi wa Serengeti Ecosystem Development and Conservation Project, unaotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Wananchi wa Ujerumani (KfW), TANAPA na FZS.
“Mwaka huu tutaendelea na usimikaji wa mabango ya matumizi ya ardhi yenye maelezo ya wajibu na katazo kwa kila eneo lililotengwa, sambamba na kupata majina ya wanavijiji 100 kutoka makundi maalum kwa ajili ya kupimiwa ardhi na kupewa hati milki za kimila bila gharama yoyote,” alisema Bi. Lucia.
Alifafanua kuwa wanufaika wa mpango huo ni wajane, walemavu, wazee, watu wenye kipato duni na wagane, ambapo watu 25 walichaguliwa mwaka 2018 na wengine 75 waliteuliwa kupitia mchakato wa mwaka 2024, wakiwakilisha vitongoji mbalimbali vilivyotoa wastani wa watu 20 kila kimoja.
Bi. Lucia aliongeza kuwa zoezi la usimikaji wa mabango linafuata matumizi yaliyopitishwa na mkutano wa hadhara, yakiwemo maeneo ya makazi, taasisi, malisho na hifadhi za mito.
Kwa mujibu wa takwimu, hadi sasa wananchi 6,369 kutoka vijiji vya wilaya ya Bariadi wamefaidika na upatikanaji wa hati milki za kimila (CCROs) kupitia ufadhili wa FZS. Hatua hiyo imesaidia kuimarisha usalama wa miliki za ardhi, kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, pamoja na kuchochea uwekezaji wa kijamii na kiuchumi katika maeneo hayo.
Kwa ujumla, jitihada hizo zinaendelea kuweka msingi imara wa matumizi endelevu ya ardhi na uhifadhi wa mazingira kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.