HALMASHAURI ZA MKOA WA SIMIYU ZAHIMIZWA KUTEKELEZA AFUA ZA LISHE
Posted on: November 14th, 2022
Halmashauri za mkoa wa Simiyu zimesisitizwa kutekeleza afua za lishe na kuhakikisha fedha zilizotengwa kwaajili ya shughuli za lishe zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Lishe Mkoa wa Simiyu Dokt. Chacha Magige alipokuwa akizungumza katika kikao cha kamati ya Lishe ya Wilaya ya Bariadi kilichofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi iliyopo Dutwa.
Dokt. Chacha alibainisha kuwa suala la lishe ni Agenda ya kitaifa kutokana na umuhimu wake hivyo katika kuandaa bajeti za halmashauri ni lazima kuhakikisha kuwa fedha ya kutekeleza shughuli mbalimbali za lishe zinatengwa na kuhakikisha fedha hizo zinatekeleza shughuli zilizopangwa.
Aidha Afisa Lishe wilaya ya Bariadi Ndg. Raphael Mtaho alibainisha miongoni mwa shughuli mbalimbali zilizotekelezwa kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 ni pamoja na kutoa matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambapo lengo lilikuwa kuwafikia watoto 376 waliofikiwa na kupewa matibabu ni watoto 373 sawa na asilimia 99.2
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 imefanya vizuri katika utekelezaji wa Afua za Lishe ikiwa imeshika nafasi ya kwanza katika Mkoa wa Simiyu huku kitaifa ikiwa nafasi ya 78 kati ya Halmashauri 180.