KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI WILAYA CHAJADILI RASIMU YA BAJETI YA 2025/2026
Bariadi, 21 Februari 2025 – Kikao cha Kamati ya Ushauri Wilaya (DCC) kimefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, kata ya Dutwa, kikiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Simon P. Simalenga, ambapo wajumbe walijadili rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Akifungua kikao hicho, Mhe. Simalenga alisema lengo kuu ni kujadili changamoto zilizopo wilayani na kuzitafutia ufumbuzi kupitia bajeti ijayo. Alisisitiza kuwa bajeti hiyo inalenga kuimarisha utawala bora, kuongeza ukusanyaji wa mapato, na kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Afisa Mipango wa Wilaya, Ndg. Raymond Kilindo, bajeti ya 2025/2026 imezingatia vipaumbele vya wilaya, ikiwemo elimu, afya, usimamizi wa fedha, na motisha kwa watumishi wa umma. Alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi inatarajia kukusanya na kutumia shilingi bilioni 34.732 kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo:
Mapato ya ndani – shilingi bilioni 2.6
Ruzuku ya mishahara – shilingi bilioni 22.9
Ruzuku ya matumizi ya kawaida – shilingi bilioni 1
Fedha za miradi ya maendeleo – shilingi bilioni 8
Katika kikao hicho, Mjumbe,Ndg. Stephen Kashinje aliuliza kuhusu utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo kwa wananchi. Akijibu swali hilo, Afisa Mipango wa Wilaya alieleza kuwa taratibu zote zimeshaainishwa kupitia vikao vya Halmashauri na Baraza la Madiwani mpaka ngazi ya kijiji. Alisema baadhi ya wananchi tayari wameshapata mikopo na kuelekeza wale wenye maswali zaidi wanaweza kufika Ofisi ya Maendeleo ya Jamii wilaya kwa maelezo ya kina.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa mapendekezo mbalimbali ya kuboresha utekelezaji wa bajeti na kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi ili kuinua maendeleo ya Wilaya ya Bariadi.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.