Pamoja na maendeleo yote ambayo nchi yetu imeyafikia, katika Afya, Elimu na Uchumi bado kuna Utapiamlo unaoendelea kuadhiri jamii ya Tanzania na hivyo kusababisha kasi ya kupunguza umaskini nchini kuwa hafifu na yakutokuridhisha.Haya aliyasema Afisa Tarafa ya Dutwa, Bi. Isabella Nyaulingo aliyekuwa akimwakilisha mgeni rasmi (Mkuu wa Wilaya ya Bariadi) katika Maadhimisho Siku ya Lishe Kitaifa yaliyofanyika uwanja wa CCM Dutwa, Wilaya ya Bariadi, tarehe 30/10/2024.
Bi. Nyaulingo alisema zaidi ya kuadhiri maendeleo ya ukuaji mwili wa mtoto,lishe duni huadhiri maendeleo ya ukuaji akili, kielimu na ubunifu wake akiwa mtu mzima.Pia hali hii huadhiri maendeleo yake binafsi na taifa kwa ujumla.
Aidha alisema tafiti mbalimbali kutoka shirika la afya duniani ( WHO) zinaonyesha watoto wenye Utapiamlo Mkali wako kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha mara 5 hadi 20 zaidi ya watoto wenye lishe nzuri.Tatizo la utapiamlo ni moja kati ya matatizo ya lishe yanayochangia magonjwa na vifo vingi kwa watoto walio chini ya miaka mitano nchini.
" Licha ya Serikali kushirikisha Wadau mbalimbali bado tatizo hili linapungua kwa kiwango kidogo hasa kwa watoto, kwa viashiria vya udumavu na pungufu wa uzito ukilinganisha na mwaka 2022.Katika Mkoa wetu udumavu ni 33%,upungufu wa uzito ni 11%, watoto kupungukiwa damu ni 28%, upungufu wa damu kwa kina mama wajawazito ni 20% na hii ni kutokana na takwimu alizotoa Afisa Lishe, hivyo hali bado si nzuri" Aliongeza Afasa Tarafa huyo.
Ameongeza kuwa kutokana na kuwepo utapiamlo,mkoa wa Simiyu umeendelea kutoa elimu kutokana na tatizo hilo na hata maadhimisho hayo yameandaliwa ili kuwakumbusha wananchi faida inayotokana kwa kula vyakula mchanganyiko.Aidha kupitia maadhimisho hayo amewahasa wananchi katika familia kutumia vyakula mchanganyiko ili kuepukana na utapiamlo na magonjwa yasiyoambukiza.
Ili kupunguza utapiamlo halmashauri ya wilaya ya Bariadi imekua ikitoa elimu kupitia vituo vya kutoa huduma ambavyo ni Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali, kufanya maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji ( SALIKI) na kutoa Elimu kupitia Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii (HW).
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.