Alfajiri na mapema, tarehe 17, Aprili 2025, Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi walianza safari yao maalum ya kujifunza na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza utalii wa ndani. Safari hiyo ilielekezwa katika Hifadhi maarufu ya Taifa ya Serengeti kupitia Lango la Ikoma, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara.
Msafara huo uliongozwa na Muongozaji wa Hifadhi ya Serengeti, Ndg. Sebastian Elias, ambaye aliwakaribisha madiwani hao kwa kuwatambulisha uzuri wa hifadhi hiyo maarufu duniani.
Ndg. Elias alieleza kuwa Serengeti ni moja ya maajabu ya dunia, inayojulikana kwa mandhari yake ya kuvutia ya savanna pana, miti ya akasia, na miamba ya asili maarufu kama kopjes ambayo wanyama hupanda kwa ajili ya kupumzika au kuotea mawindo.
Aliendelea kufafanua kuwa Serengeti ni makazi ya wanyama mbalimbali kama simba, tembo, chui, faru na duma, huku tukio la kipekee la 'The Great Migration' uhamaji mkubwa wa mamilioni ya nyumbu, pundamilia, na swala likiwa moja ya vivutio vikubwa zaidi duniani.
Mhe. Duka Mashauri Mapya diwani Kata ya Mwadobana ,alisema kuwa fursa hiyo ya kushiriki katika utalii wa ndani imewasaidia kufahamu zaidi kuhusu thamani ya hifadhi hiyo kubwa.
Alibainisha kuwa Hifadhi ya Serengeti inajivunia ukubwa wa takribani kilomita za mraba 14,763, na hivyo kuwa moja ya maeneo makubwa zaidi ya uhifadhi wa wanyamapori barani Afrika.
Serengeti, ambayo ni sehemu ya Urithi wa Dunia uliotangazwa na UNESCO, inaendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa picha, tafiti za wanyamapori, na juhudi za uhifadhi wa mazingira.
Kwa ujumla, safari hiyo imetoa mwanga mpya kwa viongozi wa Wilaya ya Bariadi juu ya umuhimu wa kuhifadhi maliasili na kukuza utalii wa ndani kama sehemu ya maendeleo endelevu ya taifa.
https://www.instagram.com/p/DInv5ZisOfQ/?igsh=MWZ5cTM2amFtMWhreg==
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.