Bariadi, 06 Agosti 2025
Mafunzo ya siku tatu kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata (ARO Kata) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 yamehitimishwa rasmi katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mafunzo, Ndg. Lameck Mkililia (ARO Kata – Masewa), aliwashukuru ARO wote kwa ushirikiano na kujituma kwao kuanzia siku ya kwanza hadi mwisho wa mafunzo.
“Nawapongeza kwa moyo wa kujitolea, kujifunza na kushirikiana katika kipindi chote cha mafunzo. Ushirikiano huu ndiyo msingi wa ufanisi katika kusimamia uchaguzi kwa haki na amani,” alisema Ndg. Mkililia.
Wakati wa mafunzo, Wawezeshaji kutoka Halmashauri waliwakumbusha ARO Kata kuendelea kujisomea Kanuni za Uchaguzi, Mwongozo wa Wasimamizi, na kuzingatia misingi ya uadilifu ili kuepuka migogoro, manyanyaso au uvunjifu wa sheria katika kipindi chote kuelekea na wakati wa uchaguzi.
Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha ARO Kata kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kuanzia maandalizi ya vituo, usimamizi wa upigaji kura hadi uhakiki wa matokeo.
“Tunategemea kuona uchaguzi wa haki, huru na wa kuaminika. Ninyi mna nafasi kubwa ya kuhakikisha hilo linatimia,” aliongeza mmoja wa Wawezeshaji.
Mafunzo yalifanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 4 hadi 6 Agosti 2025, yakihusisha mada mbalimbali za kiutendaji na mazoezi kwa vitendo.
Mwisho
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.