Simiyu, Julai 5, 2025
Takribani mifugo 326,000 tayari imechanjwa na kutambuliwa nchini tangu kuanza kwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo tarehe 2 Julai 2025.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa kampeni hiyo katika Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema hatua hiyo ni ishara ya dhamira ya Serikali katika kuboresha afya ya mifugo na kuinua thamani ya mazao yake kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
“Tayari tumefikia hatua nzuri. Tumeanza kuchanja na kutambua mifugo yetu, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha afya ya mifugo na kuvutia masoko ya kimataifa. Pia, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alishatuletea madume bora 754 yaliyosambazwa kwa wafugaji nchi nzima. Leo hii tunatekeleza haya yote huku Serikali ikigharamia utambuzi kwa kutumia hereni za kielektroniki,” alisema Mhe. Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha kuchakata nyama cha Union Meat, Bi. Ng’hwani, alisema kuwa kampeni hiyo imeongeza thamani ya nyama wanayosindika na kuongeza uaminifu wa bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.
“Mimi nilikuwa Jaji nchini Ushelisheli, lakini mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya mifugo niliyoyaona chini ya uongozi wa Rais Samia yamenisukuma kurudi na kuwekeza hapa nchini. Kupitia kampeni hii, tayari thamani ya nyama tunayozalisha imeanza kuonekana,” alieleza Bi. Ng’hwani.
Kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo ilizinduliwa rasmi tarehe 16 Juni 2025 katika Wilaya ya Bariadi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ziara ya Waziri Kijaji inalenga kufuatilia utekelezaji wa kampeni hiyo na inatarajiwa kuendelea katika mikoa ya Geita, Pwani, Morogoro, Tabora na Dodoma.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.