Bariadi, Juni 20, 2025
Akifungua kikao kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, ametoa pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2023/2024.
Mhe. Simalenga alianza kwa kumshukuru Mungu kwa afya njema na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.
"Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, nawapongeza kwa kufuata sheria na kuendelea kuwajibika katika matumizi ya rasilimali za umma," alisema Mhe. Simalenga.
Akitambua kuwa kikao hicho kimefanyika ikiwa ni siku ya mwisho ya utendaji wa Baraza la Madiwani nchini, Mhe. Simalenga aliwapongeza madiwani na watendaji wote wa Halmashauri kwa nidhamu, uadilifu, na ushirikiano wa hali ya juu alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake.
"Ni jambo la ajabu na la kuigwa – mradi unakamilika, fedha inabaki, na mtendaji anatoa taarifa mwenyewe kwa Mkurugenzi. Hili si jambo la kawaida, ni watu wa kipekee," alisisitiza.
Aidha, aliwapongeza kwa maandalizi na usimamizi bora wa ziara ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyodumu kwa siku tano, ambayo ilimfurahisha na kumgusa Mhe. Rais mwenyewe.
Katika hotuba yake ya kufunga, alieleza fahari ya Mkoa wa Simiyu kwa mafanikio ya kielimu yanayotokana na uongozi thabiti wa baraza hilo, ambalo limefanikisha Mkoa kuwa miongoni mwa mikoa mitano bora kitaifa.
"Nawatakia kila la heri katika baraza lijalo, ambapo miradi na fedha za utekelezaji zitazidi kuongezeka kwani Bariadi DC inakwenda kusimamia jimbo kiutendaji," alihitimisha.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.