Bariadi, 07 Agosti 2025 –
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Bariadi Vijijini, Bi. Beatrice Gwamagobe, leo tarehe 07 Agosti 2025 ameongoza kikao muhimu kilichowakutanisha Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wadau wa Uchaguzi, na Asasi za Kiraia kwa lengo la kuweka wazi ratiba na hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Akifungua kikao hicho kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Bi. Gwamagobe alieleza kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi kuwasilisha kwa wadau taarifa rasmi kuhusu kalenda ya uchaguzi ili kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa ratiba iliyowasilishwa:
Bi. Gwamagobe alifafanua kuwa tarehe 27 Agosti 2025 imetengwa rasmi kuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa nafasi za Rais na Makamu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Uteuzi huo utafanyika kwa siku moja na kukamilika ndani ya muda uliopangwa kisheria.
Bi. Gwamagobe alithibitisha kuwa siku ya kupiga kura kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani itakuwa Jumatano, tarehe 29 Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tume, hadi sasa wapiga kura waliokwisha jiandikisha ni 37,655,559 kote nchini, ambao wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo wa kihistoria.
Mwisho
Kwa maelezo zaidi kuhusu kalenda ya uchaguzi na taratibu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, tembelea tovuti rasmi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi www.nec.go.tz
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.