Bariadi, 08 Mei 2025 — Katika juhudi za kuboresha huduma za afya na mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa Kenani Kihongosi, amekabidhi pikipiki mbili pamoja na vifaa vya kisasa vya kielektroniki kwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Hospitali ya Wilaya ya Bariadi.
Msaada huo umetolewa na Shirika la AIDS Health Care Foundation (AHF) Tanzania, likiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuinua kiwango cha upimaji, kinga, tiba, matunzo, na elimu ya afya kwa jamii kuhusu VVU.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na televisheni moja, simu janja sita, printer moja, kompyuta mpakato moja, kompyuta ya mezani moja, pamoja na external hard disc mbili zenye uwezo wa terabaiti moja kila moja. Vifaa hivi vitatumika moja kwa moja katika kurahisisha utoaji huduma na usimamizi wa taarifa muhimu za kiafya.
Akizungumza wakati wa tukio hilo lililoshuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mheshimiwa Simon Simalenga, RC Kihongosi aliwahimiza viongozi wa halmashauri kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa kwa uangalifu na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora, hasa katika mapambano dhidi ya VVU. Vifaa hivi ni nyenzo muhimu katika kufanikisha hilo,” alisema Kihongosi.
Kwa upande wao, wakurugenzi wa halmashauri zote mbili walipokea vifaa hivyo kwa shukrani na kuahidi kuhakikisha vinatumika kikamilifu kuboresha afya ya jamii ya Bariadi.
Huu ni mfano wa ushirikiano chanya kati ya serikali na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha afya ya Watanzania inalindwa na kuimarishwa.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.