RC SIMIYU AANZA ZIARA BARIADI DC KIJIJI KWA KIJIJI
Posted on: January 9th, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Kenani Kihongosi leo Januari 09, 2025 ameanza ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Kijiji kwa kijiji ambapo kwa kuanzia ameanza Kata ya Sapiwi vijiji vya Nyamikoma, Sapiwi, Mwandama, Igegu Magharibi na Igegu kisha kumalizia Kata ya Dutwa Kijiji cha Mwamabu.
Ziara hiyo yenye lengo la kusikiliza kero na changamoto za wananchi kisha kuzipatia ufumbuzi imekuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi kwani miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa katika maeneo mengi ni changamoto ya ubovu wa barabara, changamoto ya uvamizi wa wanyamapori, changamoto ya maji na changamoto ya umeme.
Baada ya changamoto hizo kuwasilishwa Mhe.Kihongosi alizipatia ufumbuzi kupitia jopo la wataalamu kutoka Idara na taasisi mbalimbali za Serikali ambapo changamoto nyingi zilipatiwa majibu papo hapo na chache zilihitaji muda katika utatuzi wake.
"Lengo langu Mkuu wa Mkoa kuja hapa pamoja na viongozi wengine moja tujue wananchi wetu wanachangamoto gani, wananchi wetu wana kero zipi, na Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwamba 'ninawatuma muende mukaniwakilishe, wajibu wenu ni kwenda kutatua na kumaliza kero za watu' ndio maana nimefika hapa, na hii ziara nitatembelea vijiji vyote 478 vya Mkoa huu na tutavimaliza kama ambavyo tulianza kutembelea kwenye Kata". Alisisitiza Mhe.Kihongosi
Aidha katika ziara yake miongoni mwa masuala ambayo ameyasisitiza ni pamoja na kudumisha amani na mshikamano huku akiwasihi wananchi kutokubali kugawanyika kwa sababu za kisiasa.
Ziara ya Mhe.Kihongosi kutembelea kila kijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi itaendelea siku ya kesho tarehe 10 Januari 2025 huku wananchi wakiombwa kujitokeza kwa wingi ili kuwasilisha kero na changamoto zinazowakabili.