RUWASA SIMIYU YATIA SAINI MIKATABA YA UJENZI WA MIRADI YA MAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023
Posted on: January 11th, 2023
Wakala wa maji na Usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) mkoa wa Simiyu imetia saini mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji inayotarajiwa kutekelezwa kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023.
Akieleza katika Hafla fupi ya utiaji saini Meneja wa RUWASA mkoa wa Simiyu Mhandisi Mariam Majala amebainisha kuwa kwa mwaka huu wa fedha wanatarajia kutekeleza miradi 15 ya maji bomba ikiwa miradi 10 kati ya hiyo itatekelezwa Wilaya ya Bariadi, mradi 1 wilaya ya Busega, mradi 1 wilaya ya Itilima, miradi 2 wilaya ya Maswa na mradi 1 wilaya ya Meatu.
Vilevile RUWASA mkoa wa Simiyu inatarajia kuchimba visima virefu 28, Wilaya ya Bariadi visima 10, wilaya ya Itilima visima 4, Wilaya ya Maswa visima 10 na Wilaya ya Meatu visima 4. Pia inatarajia kufanya ukarabati wa Pampu za mkono 370.
Meneja huyo alifafanua kuwa miradi hiyo ipo katika hatua za mwisho za manunuzi na tayari mikataba ya ujenzi wa miradi 8 imekamilika na utiaji saini ndio umefanyika leo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mh.Dokt. Yahaya Nawanda ambaye alishuhudia utiaji saini huo licha ya kutoa Shukrani zake za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dokt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo lakini aliwataka wakandarasi wote watakaotekeleza miradi hiyo kutekeleza kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, aidha Mh. Nawanda aliwasisitiza kuwa Viongozi wa Mkoa na Wilaya hawatamvumilia mkandarasi yeyote atakayetekeleza miradi hiyo chini ya kiwango au kuchelewesha.
“Sisi Mkoa wetu tunataka miradi mizuri, tunataka tusimamie fedha za serikali vizuri ili mwisho wa siku wananchi wanufaike na fedha zao” alisisitiza Dokt. Nawanda
Miongoni mwa miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ni miongoni mwa Halmashauri zitakazonufaika na miradi hiyo ambapo kata za Ngulyati, Sakwe, Mwadobana, Sapiwi, Mwaubingi na Matongo zinatarajia kupata miradi.