SIMIYU YAWEKA MIKAKATI YA KUBORESHA ELIMU NA UFAULU ENDELEVU
Posted on: February 11th, 2025
Katika kuendeleza juhudi za kupandisha ufaulu wa wanafunzi Mkoa wa Simiyu umeweka mikakati mbalimbali ambayo itasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za kielimu kwa kuzingatia vigezo vya upimaji, Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu Ndg.Khalifa Shemahonge amebainisha kuwa miongoni mwa mikakati ambayo Mkoa umeweka ni pamoja na kuchochea Ari ya utendaji kazi kwa walimu, utoaji wa chakula shuleni, kusimamia ufundishaji fanisi, kuanzisha kambi salama za taaluma pamoja na uboreshaji wa miundombinu na samani.
Aidha Afisa Elimu huyo alisisitiza ili wanafunzi waweze kufaulu vizuri katika mitihani yao ni lazima jamii na wadau wote wa elimu kila kundi liweze kutimiza wajibu wake, baadhi ya wadau hao ni pamoja na walimu, wazazi, viongozi wa Serikali za vijiji na kata na hata viongozi wa kimila.
"Nenda kaikamate jamii, huwezi kuchomoka peke yako hata siku moja, kaondoe ugomvi wako na Mtendaji wa Kata, kaondoe ugomvi wako na viongozi wa dini, kaondoe ugomvi wako na viongozi wa kisiasa" alisisitiza Afisa Elimu huyo.
Aidha katika kikao kazi hicho Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ilipongezwa kwa kuongoza kimkoa katika matokeo ya Kidato cha Nne na darasa la Saba, mathalani Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi jumla ya wanafunzi 4,951 wamefaulu mtihani huo sawa na asilimia 85.