TATIZO LA UKATIKAJI UMEME BARIADI MBIONI KUTATULIWA
Posted on: December 17th, 2024
Katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika eneo la Imalilo, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu ambapo kituo hiki kinatarajiwa kuwa suluhu ya tatizo la ukatikaji wa umeme katika Wilaya ya Bariadi.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi Bilioni 75 unahusisha ujenzi kituo cha kupoza umeme wa KV 220 mradi ambao utatekelezwa kwa kipindi cha muda wa miezi 18 ambapo kwa sasa mkandarasi bado yupo eneo la mradi na punde taratibu za malipo yake zikikamilika ataendelea na utekelezaji wa mradi huo.
Afisa uhusiano na huduma kwa wateja wa TANESCO Mkoa wa Simiyu Bi. Adelina Lyakurwa akiwasilisha taarifa yake katika kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya ya Bariadi kilichofanyika Disemba 17, 2024 alieleza kuwa katika Wilaya ya Bariadi kuwa vijiji vyote 84 vimesambaziwa umeme na vitongoji 194 kati ya 512 vimesambaziwa umeme pia katika mwaka huu wa fedha vitongoji 15 vinatarajiwa kunufaika na mradi wa ujazilizi ambao una lengo la kuongeza mtandao wa umeme katika ngazi ya vitongoji.
Aidha Bi.Adelina alieleza kuwa kwa sasa jitihada mbalimbali zinaendelea kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana katika majira yote na miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kubadilisha nguzo za miti na kuweka nguzo za zege ambazo ni imara na zinastahimili hali zote.
Mwisho Bi. Adelina alitoa rai kwa jamii kuepuka wizi wa miundombinu ya umeme kwani kufanya hivyo kunakwamisha juhudi za serikali katika kutatua changamoto za umeme kwa wananchi.