Kamati ya Elimu, Afya na Maji ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, tarehe 22 Januari 2025, ilifanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Jengo la kuhifadhi Maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya afya kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Mganga Mfawidhi wa Wilaya, Ndg. Magembe Kuligwa Pelana, alieleza kuwa kiasi cha shilingi milioni 172 kilitolewa kwa hospitali hiyo ili kukamilisha Jengo la kuhifadhi Maiti, Jengo la Upasuaji, na Wodi ya Watoto. Kati ya fedha hizo, shilingi 73,541,512.88 tayari zimetumika katika ujenzi wa Jengo la Kuhifadhi Maiti.
Mradi huo, unaosimamiwa na mkandarasi, umefikia hatua za mwisho, ikiwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya maji safi, maji taka, umeme, na kufunga milango pamoja na madirisha ya vioo. Kukamilika kwa ujenzi kunatarajiwa ifikapo tarehe 2 Februari 2025, ambapo huduma za kuhifadhi maiti zitaanza kutolewa rasmi.
Kamati hiyo ilitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa za serikali katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inafanikishwa. Aidha, walimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg. Halidi M. Mbwana, pamoja na wataalamu wengine kwa kujituma katika kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa jamii.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imeidhinisha shilingi milioni 472 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo. Hatua hii inatoa matumaini makubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Bariadi katika kupata huduma bora za afya.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.