Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi imeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa shule mbili za sekondari katika kata ya Nkololo ambapo moja ya shule hiyo inarajiwa kufundisha Elimu ya Amali ambayo huwa na michepuo kama vile Kilimo na Ufugaji, Umakenika, Sanaa bunifu, Michezo na Urembo.
Ujenzi wa shule hizo unatekelezwa kupitia mradi wa SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 584 kwa kila shule ambapo kukamilika kwa shule hizo kutasaidia kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi wanaodahiliwa katika Shule ya sekondari Nkololo.
"Kwa Muhula mpya wa masomo mwaka 2025 wanafunzi wa kidato cha kwanza 641 wamechaguliwa kujiunga na masomo katika Shule ya Sekondari Nkololo, idadi hii ya wanafunzi ni kubwa kutokana na Kata nzima ya Nkololo kuwa na Shule ya Sekondari moja" alifafanua Mwl. Joseph Cheyo , Mkuu wa shule ya Sekondari Nkololo.
Ujenzi wa shule hizi ni utekelezaji wa mpango wa Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia ambapo kupitia miradi mbalimbali Serikali imekuwa ikijenga miundombinu kama vile madarasa, maabara, nyumba za walimu au shule ili kila mtoto apate haki ya kupata elimu iliyo bora.