Bariadi, 04 Agosti 2025 – Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi imeendesha zoezi la kuwaapisha rasmi Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata (ARO Kata) kama sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Shughuli hiyo muhimu imefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri na kuongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa, ambapo wasimamizi wote walitoa kiapo cha uaminifu na uadilifu mbele ya mamlaka ya kisheria.
Katika hotuba yake, Mhe. Kiliwa aliwataka wasimamizi hao kuwa waaminifu, waadilifu na kutoegemea upande wowote katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi. Aidha, aliwakumbusha kufuata kikamilifu kanuni, taratibu na miongozo ya uchaguzi ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wenye kuaminika.
Kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu ni:
“Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura”
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi inawataka wananchi wote kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kutumia haki yao ya kupiga kura, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha misingi ya utawala bora na demokrasia nchini.
> Tunaendelea kuandaa mazingira salama na rafiki kwa kila mpiga kura ili kuhakikisha kila sauti inasikika.
Mwisho
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.