Bariadi, 04 Agosti 2025
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Bariadi Vijijini, Bi. Beatrice Gwamagobe, kwa niaba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), amewapongeza Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata (ARO Kata) kwa kuaminiwa na kuteuliwa rasmi kusimamia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa viapo vya uaminifu na utekelezaji wa majukumu yao, Bi. Gwamagobe aliwakumbusha ARO Kata hao kuwa uteuzi wao umezingatia masharti ya Kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, ambayo inaweka msisitizo kwenye sifa za uadilifu, uaminifu, uzalendo na uchapakazi.
Aidha, alisisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu yao unatakiwa kuendana na masharti ya Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inatambua kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
“Kwa kuzingatia niliyoeleza awali, nyinyi mliopo hapa mmeteuliwa kwa mujibu wa sheria, na tangu tarehe ya uteuzi wenu mnao wajibu wa kikatiba na kisheria wa kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa niaba ya Tume, katika maeneo yenu ya uteuzi,” alieleza Bi. Gwamagobe.
Uteuzi wa ARO Kata ni hatua muhimu katika maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kwa uwazi, haki na amani. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kuimarisha misingi ya demokrasia kwa kuhakikisha kila hatua ya maandalizi ya uchaguzi inazingatia sheria na taratibu za nchi.
Kwa mwaka 2025, Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya Majimbo ya Uchaguzi 264, ikiwa ni Tanzania Bara (214) na Zanzibar (50).
Maandalizi katika kila jimbo yanaendelea kuratibiwa kwa weledi na uwazi.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.