Wataalamu wa Kamati ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wamepatiwa mafunzo kuhusu namna ya kuandaa miradi kwa mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Mafunzo hayo yalitolewa jana, Februari 13, 2025, na wawakilishi kutoka Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), wakiongozwa na Dr. Edward Makoye na Ndg. Jones Mwalemba.
Lengo la mafunzo hayo lilikuwa kuwaelimisha wataalamu wa Halmashauri juu ya miongozo mbalimbali ya ufadhili wa miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na sekta binafsi. Akizungumza katika mafunzo hayo, Dr. Edward Makoye alieleza kuwa sekta binafsi inaweza kushiriki katika utekelezaji wa majukumu ya serikali kwa njia mbalimbali, zikiwemo ujenzi wa miundombinu mipya na kuiendesha kwa niaba ya serikali,utoaji wa huduma kwa kutumia miundombinu ya serikali iliyopo na ukarabati pamoja na uendeshaji wa miundombinu ya serikali kupitia makubaliano maalum.
Katika mafunzo hayo, Dr. Makoye alitaja miradi kadhaa inayotekelezwa kwa mfumo wa PPP, ikiwemo Expressway ya Tozo kutoka Kibaha hadi Dodoma, Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (DART) awamu ya 1-6, na ukarabati wa miundombinu ya reli ya TAZARA.
Kwa mujibu wa sheria ya PPP, miradi inaweza kutekelezwa kupitia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na serikali kuibua na kuandaa miradi kabla ya kushirikisha sekta binafsi, mwekezaji binafsi kuibua mradi na kugharamia andiko lake kwa ajili ya kutekelezwa kwa ubia na serikali, majadiliano ya moja kwa moja kati ya serikali na mwekezaji binafsi mwenye sifa zinazokidhi vigezo vya mradi husika na pia serikali inaweza kushirikiana na sekta binafsi katika miradi iliyoibuliwa, ambapo uidhinishaji wake hufanywa na Baraza la Mawaziri baada ya kupokea ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mafunzo hayo pia yalitoa fursa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kuwasilisha miradi yao inayopangwa kutekelezwa kwa mfumo wa PPP. Mkuu wa Kitengo cha Mipango Wilaya, Ndg. Raymond Kilindo, alibainisha kuwa Halmashauri tayari imeandaa maandiko kwa ajili ya miradi sita, ambapo miradi minne imechaguliwa kwa utekelezaji wa awali. Kwa sasa, taratibu za kuandaa maandiko kwa ajili ya utekelezaji wake zimeanza kwa kushirikiana na wataalamu kutoka PPPC.
Akizungumzia umuhimu wa PPP, Dr. Makoye alisema kuwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi unaleta faida nyingi, zikiwemo kuongeza ujuzi na ubunifu hasa katika teknolojia, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kuongeza rasilimali fedha, na kuhakikisha mali za serikali zinatunzwa ipasavyo.
Mafunzo hayo yameleta mwanga kwa wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi juu ya fursa zilizopo katika mfumo wa PPP, huku matarajio yakiwa ni kutekeleza miradi ya maendeleo kwa njia bora zaidi kwa manufaa ya wananchi.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.