WATENDAJI WAPEWA MAFUNZO YA MFUMO WA UKUSANYAJI WA TAKWIMU ZA MAJENGO
Posted on: April 14th, 2025
Watendaji wa Kata na vijiji kutoka Kata tatu za Nkololo, Dutwa na Sapiwi jana Aprili 14, 2025 wamepewa mafunzo juu ya matumizi ya mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za majengo ambao unalengo la kukusanya taarifa za majengo ili kuwezesha ukusanyaji wa kodi ya majengo.
Akifafanua wakati wa mafunzo hayo mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Francis Johanes amebainisha viwango vya kodi hizo kuwa, nyumba ya kawaida isiyo ya ghorofa kwa mwaka ni shilingi 18,000 na kwa majengo ya ghorofa kila sakafu (floor) moja ni shilingi 90,000 kwa mwaka.
Aidha mwezeshaji huyo alibainisha kuwa yapo majengo mbalimbali ambayo sheria imetoa msamaha wa kodi hiyo, miongoni mwa majengo hayo ni pamoja na; majengo ya serikali yanayotumika kwa matumizi ya umma, majengo ya taasisi za dini ambayo hayatumiki kibiashara na kujipatia kipato, majengo yanayomilikiwa na asasi zisizo za kiserikali ambayo hayatumiki kibiashara pamoja na nyumba za tope, nyumba zilizojengwa na miti na udongo ambazo hutumika kwa makazi.
Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hili ambalo linatarajiwa kuanza kata za Dutwa, Nkololo na Sapiwi kuanzia tarehe 15 Aprili, 2025. Aidha wananchi wanakumbushwa kuwa ukusanyaji wa kodi hii kwa mfumo wa LUKU utaendelea kutumika kwa walipa kodi wenye mita za umeme na kwa walipa kodi wasio na mita za umeme mfumo wa TAUSI utatumika kukusanya kodi hiyo ambapo wateja hao watatumiwa ankara za madai kulingana na viwango vilivyobainishwa kwa mujibu wa sheria.