Bariadi, 16 Julai 2025 – Watumishi wapya wa umma, wengi wao wakiwa ni walimu pamoja na watumishi kutoka idara mbalimbali, leo wamepatiwa semina kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma na Uwajibikaji kazini. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Bariadi, Ndg. Wang’engi M. Mohabe, alieleza kuwa ili mwalimu athibitishwe kazini ni lazima awe amemudu majukumu yake kikamilifu katika kipindi cha matazamio.
“Baada ya tathmini ya utendaji wa mwalimu katika kipindi cha miezi 12, Katibu Msaidizi huwasilisha mapendekezo ya mwajiri kwenye kikao cha Kamati ya Wilaya ambayo huamua kama mwalimu athibitishwe, apewe muda zaidi wa kujirekebisha au ajira yake isitishwe,” alisema Mohabe.
Aidha, alibainisha kuwa sifa zinazozingatiwa katika upandishaji wa cheo kwa mwalimu ni pamoja na utendaji bora wa kazi, kiwango cha elimu, muundo wa kada, nafasi ya kazi, cheo cha awali, bajeti ya mwajiri na idadi ya watumishi (ikama) iliyoidhinishwa.
Kuhusu masuala ya kinidhamu, Mohabe alifafanua kuwa Wakuu wa Shule ni mamlaka ya kwanza ya kinidhamu kwa walimu katika ngazi ya shule, huku Tume ya Utumishi wa Walimu ngazi ya Wilaya ikiwa ni mamlaka ya rufaa kwa walimu wasioridhika na maamuzi hayo.
“Walimu wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa makosa kama vile utoro wa siku tano mfululizo, wizi, ubadhirifu wa mali za umma, kuchelewa kazini, matumizi mabaya ya rasilimali, ugomvi kazini, uchonganishi, ulevi, na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Wilaya ya Bariadi, Ndg. Hassan Malingumu, aliwaeleza washiriki kuhusu haki za msingi za watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kulipwa mshahara, posho ya kujikimu, fidia endapo kuna ajali au kifo kazini, uhamisho na likizo.
Semina hiyo iliandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao wapya kuhusu wajibu, haki, na mipaka yao katika utumishi wa umma. Mada mbalimbali ziliwasilishwa na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo TSC, Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Uthibiti Ubora wa Elimu na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bariadi, katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, Halmashauri ilipokea Kibali Na. FA.97/288/01/09 cha tarehe 25 Juni 2025, cha kupangiwa watumishi kutoka kada mbalimbali. Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2025, jumla ya watumishi wapya 45 walikuwa wameripoti kazini, huku taratibu za kiutumishi zikiendelea.
Bariadi
Anuani: 109-Bariadi
Simu: 028 2700012
Simu: +255683705815
Barua Pepe: info@bariadidc.go.tz
Copyright ©2019 Bariadi District Council . All rights reserved.